Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, kikao cha kielimu maalumu kwa wanawake wa Kishia kilifanyika katika mji wa Yangon nchini Myanmar. Lengo kuu la kikao hiki lilikuwa ni kuinua uelewa wa kidini kwa wanawake na kuimarisha nafasi yao ndani ya familia na jamii. Msingi wa kikao hiki uliwekwa juu ya mafundisho ya Qur’ani Tukufu na mwenendo wa Ahlul-Bayt (a.s), na kikao hiki kilitoa fursa muafaka ya majadiliano na kubadilishana mawazo kuhusu nafasi ya wanawake katika kuimarisha familia na kutekeleza majukumu ya kijamii.
Mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (a.s)
Katika kikao hiki, Zaynab Madina Beg, mhubiri wa dini, katika hotuba yake yenye mada isemayo “Mfano wa kuigwa wa Bibi Fatima (a.s)”, alisisitiza kwamba mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (a.s) hata leo bado ni mfano kamili na wa kivitendo kwa wanawake, na kwamba ibada, majukumu ya kifamilia, uelewa wa kijamii na ukweli katika maneno ni mihimili ambayo kila mwanamke Mwislamu anaweza kwa kuifuata kujenga jamii iliyo bora zaidi kiakili na kimaadili. Aliongeza kuwa; iwapo wanawake wataupanga mwenendo wa maisha yao kwa kuzingatia sira ya Bibi Fatima (a.s), jamii itaelekea kwenye uimara wa fikra na maadili.
Mfano bora wa haya, maadili na usafi wa maadili
Katika kuendelea kwa kikao, Bi Sayyida Mehrin Husseini, katika hotuba yake, alimwasilisha Bibi Fatima Zahra (a.s) kama mfano bora wa haya, maadili na usafi wa maadili katika historia ya Uislamu, na akasisitiza kwamba usafi wa maadili si sifa ya mtu binafsi pekee, bali ni nguzo kuu ya kuundwa kwa jamii ya Kiislamu iliyo hai na yenye afya. Aliongeza kuwa; wanawake wa leo wanapaswa kuukubali usafi wa maadili kama utambulisho wao na kama nguvu yenye uwezo, na wautumie katika safari yao ya maendeleo ya binafsi na ya kijamii.
Maisha mema (Hayatu Twayyiba)
Baadaye, Bi Sayyida Radhia Husseini alizungumzia mada ya maisha mema na kubainisha kuwa; Uislamu unawawezesha wanawake kutekeleza majukumu yao ya kijamii kwa heshima, uwajibikaji na ukuaji wa kiroho. Alisisitiza kuwa kufikia maisha mema kunawezekana tu pale ambapo wanawake, sambamba na kushikamana na maadili ya kidini, wanatekeleza pia majukumu yao ya kijamii kwa uelewa na utambuzi kamili.
Mbinu za malezi kwa wanawake
Katika sehemu ya mwisho ya kikao, Sayyida Nazira Husseini aliwasilisha makala ya utafiti kuhusu mbinu za malezi kwa wanawake, na kutoa mapendekezo ya kielimu na ya kivitendo kwa ajili ya kuimarisha elimu na uelewa wa wanawake katika jamii. Uratibu na usimamizi wa masuala ya kiutendaji ya kikao pia ulifanywa na Mheshimiwa Zaynab Madina Beg kwa ufanisi mkubwa, na hivyo kuwezesha kufanyika kwa kikao kilichoandaliwa vyema na chenye athari chanya.
Washiriki wa kikao hiki walieleza kuwa kikao hicho kilikuwa na mchango mkubwa katika kuinua fikra, uelewa wa kidini na nafasi ya kijamii kwa wanawake, na wakaonesha matumaini kwamba kuandaliwa kwa vikao kama hivi vya kielimu nchini Myanmar kutachangia kwa kiasi kikubwa katika kueneza haki za wanawake, kuimarisha maadili ya kifamilia, na kuundwa mshikamano na maelewano ya kijamii.
Kikao hiki hakikuwa tu fursa ya kuongeza uelewa wa kidini kwa wanawake, bali pia kilikuwa jukwaa muafaka la kubadilishana uzoefu, kuinua ujuzi wa kijamii, na kuwahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika jamii ya Kiislamu.
Maoni yako